keeping you up-to-date
Chadama Ni Hatari

Siasa za kushutumiana, kupakana matope zimeendelea kutawala kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha na safari hii, wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Akeri, wakiwalalamikia walimu wa shule za msingi na sekondari kwamba wamekigeuka chama hicho na kushabikia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuwafundisha wanafunzi wao kutumia msemo unaotumiwa na Chadema wa 'people’s power'

Kadhalika, wazee hao wamelaani wafuasi wa Chadema, kwa kupiga yowe kwenye mikutano ya kampeni na kila wanapoona wafuasi wa CCM waliovalia sare za chama.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika tawi la CCM la Patandi lililopo eneo la Tengeru, wazee hao walisema jana kuwa mila na desturi za Kimeru zinazua yowe kupigwa bila sababu hasa kama hakuna msiba, lakini inashangaza kuona kwamba hata watoto wadogo wanapiga yowe na kuonyesha alama ya vidole viwili pindi wanapoona wafuasi wa CCM.

Mweyekiti wa Jumuiya ya wazazi wa CCM Kata ya Akeri, Ndewariyo Kaaya, alisema: “Inasikitisha kwamba hadi watoto wadogo wa shule wakiona mtu amevaa nguo zetu (CCM) wanapiga yowe kitu ambacho ni kibaya kwani ni uchuro na ni laana mbaya sana, labda pengine serikali yetu itusaidie.”

“Tunatukanwa hadi na watoto wadogo kabisa, ukipita wanasema ‘people’s power’ na kuonyesha vidole viwili,” aliongeza mzee huyo.

Mzee Benard Kaaya, mjumbe wa Kamati ya Siasa katika kata hiyo, alisema sehemu kubwa ya watu wanaopiga yowe ni vijana pamoja na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na kuwataka wazazi wawakanye watoto wao kushiriki jambo hilo.

“Walimu tena hapa sekondari ya Akeri, badala ya kuwafundisha watoto wetu masomo, wanawafundisha ‘people’s power’, wanawafundisha siasa, hebu tukemee vitendo hivi jamani, nawaomba mabalozi mliopo hapa tusiruhusu yowe tena kwenye kata yetu,” alisema Mzee Kaaya na kuongeza: “Hata leo asubuhi watoto wadogo wamenionyesha alama ya Chadema.”

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) tawi la Akeri, Luyana Sikawa, alisema: “Hawa walimu wamesahau kwamba wapo kwenye ajira ya CCM, wametugeuka na hawapo kabisa na sisi, hili ni jambo baya sana.”

Alimlaani mgombea wa Chadema, Joshua Nassari, kwa kutangaza kwamba atafuta ushuru unaolipwa mara mbili mbili kwenye soko la Tengeru akieleza kwamba tangazo lake limeibua vurugu sokoni hapo.

“Mgombea wa Chadema asilete vita pale sokoni, amekuwa akitangaza kufuta ushuru kitu ambacho hakiwezekani, yeye ametamka pale sokoni matokeo yake nimekuwa nikizomewa kila mahali ninapopita, watu wananipigia yowe kila wanaponiona,” alisema Sikawa, ambaye pia ni mwenyekiti wa soko hilo

Posted by admin at Mar 25, 2012 3:25 PM Category: Tanzania
Tags: